Pin It

Tembo, faru wana haki ya kuishi

“KWA mpango mkakati wa kitaifa wa kupambana na ujangili, tuamini kwamba ujangili unaendelea kudhibitiwa na katika kipindi cha miaka 15 mata...

“KWA mpango mkakati wa kitaifa wa kupambana na ujangili, tuamini kwamba ujangili unaendelea kudhibitiwa na katika kipindi cha miaka 15 matarajio ni Tanzania kuwa na tembo zaidi ya 100,000,” hayo yalisemwa na aliyekuwa Waziri wa Maliasili na Utalii wa Serikali ya Awamu ya Nne, Lazaro Nyalandu wakati wa kuzindua mkakati huo.
Mkakati huo uliozinduliwa mwaka 2014, uko katika utekelezaji huku kukiwa na taarifa za kukithiri kwa ujangili, baada ya kufanyika ya sensa ya serikali iliyobainisha kupotea kwa asilimia 60 ya tembo katika miaka mitano iliyopita.Agosti 2016, Waziri wa Maliasili na Utalii, Profesa Jumanne Maghembe alizindua kitabu cha kulinda tembo na faru akisema Tanzania ni nchi ya pili kwa kuwa na hifadhi nzuri na bora ikiifuatia Brazil na kusisitiza umuhimu wa watanzania kutunza rasilimali hizo.
Kitabu cha “Tembo-Faru wana haki ya kuishi Tanzania” kimetayarishwa na kamati ya Amani ya Viongozi wa Dini Mkoa wa Dar es Salaam kikiwa na lengo la kuwaelimisha umuhimu wa kutunza mazingira na viumbe vilivyopo kwa faida yao na vizazi vijavyo.Maghembe anasema wanyamapori ni muhimu katika maisha ya kila Mtanzania na maendeleo ya Taifa kwani sekta ya utalii inachangia asilimia 17.5 ya pato la taifa na asilimia 25 ya mapato yote ya fedha za kigeni.
Anasema mtandao wa ujangili ni mkubwa na unahusisha makundi mbalimbali yakiwemo ya watengenezaji wa silaha, waagizaji wa meno ya tembo, wasambazaji na watu ambao nyumba zao hutumika kuhifadhi na kununua meno ya tembo. Ripoti ya sensa ya tembo ya mwaka 2014 inaonesha kuwa tembo 65,721 wamekufa ndani ya miaka mitano iliyopita na kufanya idadi yao kupungua kutoka 109,051 waliokuwapo mwaka 2009 hadi 43,330 mwaka 2014.
Sensa hiyo ilifanywa katika eneo la kilomita za mraba 268,692 ambazo ni sawa na asilimia 28.3 ya eneo lote la nchi. Maeneo yaliyofanyiwa sensa ni Serengeti (Mara), Tarangire (Manyara), Katavi(Rukwa), Burigi (Biharamulo), Malagarasi-Muyovosi, Seolus-Mikumi na Ruaha-Rungwa, Mkomazi na Saadani.
Taarifa iliyotolewa mwaka jana na aliyekuwa Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Dk Adelhelm Meru inasema idadi ya tembo waliokuwepo wakati akitoa taarifa hiyo inajumuisha tembo zaidi ya 10,000 wa ikolojia ya Ruaha- Rungwa walioelezwa kutojulikana walipo jambo lililoilazimu serikali kufanya upya sensa ya wanyama hao. Kupotea kwa tembo hao kulifanya idadi yao katika Hifadhi ya Ruaha- Rungwa kupungua kutoka 20,000 mwaka 2013 hadi 8,272 mwaka 2014.
Wakati tembo hao wakiendelea kutafutwa, taarifa ya mwaka 2015 iliyotolewa na Nyalandu inaonesha katika Pori la Akiba la Selous lenye ukubwa wa kilomita za mraba 55,000 idadi ya tembo iliongezeka kutoka 13,000 mwaka 2013 hadi 15,217 mwaka 2014, ongezeko ambalo ni zaidi ya tembo 2,000. Katika ikolojia ya Serengeti kuna ongezeko la asilimia 98 la tembo kutoka 3,068 mwaka 2009 hadi 6,087 mwaka 2014 huku ikolojia ya Tarangire- Manyara kukiwa na ongezeko la asilimia 64 kutoka tembo 2,561 mwaka 2009 hadi 4,202.
Hifadhi ya Taifa ya Kisiwa cha Kibondo ilikuwa na tembo 49 mwaka 2009, lakini hadi mwaka 2014 ilikuwa na tembo 102, wakati Hifadhi ya Taifa ya Arusha ilikuwa na ongezeko la tembo kwa asilimia 100, kutoka tembo 100 mwaka 2009 hadi 200 mwaka 2014.
Katika ikolojia ya Katavi-Rukwa, tembo wameongezeka na kufikia 6,400, Malagarasi-Muyovosi kulikuwa na tembo 15,198 mwaka 2009 lakini walipungua hadi 2,953 mwaka 2014, wakati Hifadhi ya Taifa ya Kilimanjaro kulikua na tembo 45 mwaka 2009, waliongezeka hadi kufikia tembo 100 mwaka 2014. Ripoti ya mwaka 2014 ambayo ililenga kuangalia kiwango cha uhalifu, ufisadi na kuangamizwa kwa tembo, Shirika la Upelelezi wa Mazingira (EIA) lilibainisha kuwa tembo wa Tanzania wanauawa ili kutosheleza biashara ya pembe za ndovu nchini China na zile za bara la Asia.
Kati ya mwaka 1977 na 1987, utafiti wa shirika hilo unaonesha, Tanzania ilipoteza tembo 50 ambayo ni sawa na asilimia 50 ya idadi ya tembo wote. Mwaka 1989, Tanzania ilipendekeza marufuku ya kimataifa ya biashara ya pembe za ndovu wote wa Afrika baada ya kubaini isingeweza kukabiliana na janga hilo peke yake. Marufuku hiyo iliyodumu kwa muongo mmoja iliifanya Tanzania ipongezwe na jumuiya ya kimataifa kama mtetezi wa tembo wa Afrika.
Mkurugenzi wa EIA Mary Rice ananukuliwa akisema, tatizo la ujangili lilidhibitiwa na idadi ya Tembo ilirejea na hali yake kuimarika. Kwa mujibu wa EIA, viashiria vyote vya ujangili vilivyoleta wasiwasi miaka ya 1980 vilirudi tena na tembo wa Tanzania wakaanza kuuawa kwa wingi ili kukidhi mahitaji ya biashara ya pembe za ndovu iliyochipuka. Ingawa ongezeko la ujangili lilianza 2009, ushahidi unaonesha kwamba hali hiyo ilianza kuimarika miaka minne kabla; kati ya mwaka 2009 na 2013, idadi ya tembo iliporomoka sana.
Mwaka 2013 peke yake, taarifa ya EIA inaonesha Tanzania ilipoteza zaidi ya tembo 10,000, ikiwa ni wastani wa tembo 30 kila siku. Mkurugenzi Mtendaji wa EIA, Rice anasema tembo wa Tanzania wanaendelea kuwindwa na majangili ili kutosheleza mahitaji ya soko la magendo la pembe za ndovu hususan Uchina. Anasema takwimu za pembe zilizonaswa zinaihusisha Tanzania na idadi kubwa ya pembe zinatoka nchini kuliko nchi nyingine yoyote
. Pia inahusishwa mara kwa mara na uhalifu unaohusu shehena kubwa za pembe za ndovu zilizonaswa sehemu mbalimbali kama Hong Kong, Vietnam, Ufilipino, Malaysia, Sri Lanka na Taiwan. Akibainisha mikakati inayoendelea kuchukuliwa ili kudhibiti ujangili nchini, Prof Maghembe anasema; “serikali kwa kushirikiana na wadau imeongeza nguvu katika vita hiyo ili kumaliza ujangili.”
Akipokea msaada wa magari 21 yenye thamani ya dola za Marekani laki 6 yaliyotolewa na Taasisi ya Frankfurt Zoological ya Ujerumani, Septemba 2016, Maghembe alitangaza operesheni tokomeza ujangili. Magari hayo yalitolewa kwa ajili ya kuimarisha ulinzi na doria, ikiwa ni njia ya kupambana na ujangili dhidi ya tembo na wanyamapori wengine kama faru.
Katika mapambano dhidi ya ujangili wa wanyamapori ndani na nje ya maeneo ya hifadhi, taarifa ya wizara hiyo inaonesha kati ya mwaka 2006 na 2014, Serikali iliendesha doria zilizowezesha kukamatwa kwa watuhumiwa 17,084 na silaha za aina mbalimbali 4,111. Taarifa hiyo inaonesha kesi 6,803 zilifunguliwa katika vituo mbalimbali na kati yake, kesi 2,734 zenye watuhumiwa 2,246 zilimalizika kwa watuhumiwa kutozwa faini ya jumla ya Sh milioni 652.3 na watuhumiwa 210 walihukumiwa vifungo jela.
Akifafanua mikakati endelevu ya kudhibiti ujangili, Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Hifadhi za Taifa (TANAPA), Allan Kijazi anasema ujangili unaendelea kudhibitiwa kwa kupitia pia mradi wa ujirani mwema na vijiji vilivyopo kandokando ya hifadhi hizo ambao uhusisha ujenzi wa barabara, shule, zahanati, miradi mbalimbali ya vijiji na kuwajengea wananchi uwezo wa kiuchumi.
Mbali na operesheni mbalimbali ikiwemo ile ya Tokomeza Ujangili ya mwaka 2013 zilizofanywa na serikali kwa lengo la kuukabili ujangili, Kijazi anasema kwa kupitia mradi wa Kuboresha Maeneo Yaliyohifadhiwa Kusini mwa Tanzania (SPANEST), TANAPA imetoa namba ya simu ya bure inayotumika kupokea taarifa zinazofichua ujangili. Namba hiyo ni 0800751212. Wakati mradi wa ujirani mwema ukiimarishwa, anasema mafunzo ya askari wa wanyamapori yanazidi kutolewa, sambamba na msaada wa magari kwa ajili ya doria.
“Kupitia mradi wa Spanest (Kuboresha Maeneo Yaliyohifadhiwa Kusini mwa Tanzania) iliwakutanisha wajumbe wa kikosi kazi na wawakilishi kutoka vyombo vya ulinzi na usalama mkoni Iringa ili kuweka mikakati ya pamoja ya kuboresha ushiriki katika usimamizi wa rasilimali na kukabiliana na ujangili,” anasema. “Lakini pia tumepokea na tunaendelea kupokea msaada wa fedha na vifaa mbalimbali vinavyosaidia kupambana na ujangili kutoka kwa watu, mashirika na taasisi mbalimbali za ndani na nje ya nchi kwa ajili ya kazi hiyo,” anasema.
Anapozungumzia mchango wa jamii ya kimataifa katika uhifadhi, Prof Maghembe anasema haina budi iendelee kuwaunga mkono kifedha na kiufundi kwa kipindi kirefu kijacho ili washinde vita hiyo. Kwa kushirikiana na wadau katika kipindi cha 2014 na 2015 serikali ilipata magari, ndege, helikopta, silaha, vifaa vya askari kama mahema na kamera maalum, ikiwa ni hatua ya kuongeza nguvu kwa askari na vyombo vingine vya ulinzi na usalama katika vita hiyo.
Novemba, 2015, UNDP na GEF kwa kupitia mradi wa SPANEST, iliiwezesha taasisi ya World Elepahant Centre (WEC) kuwavalisha shingoni tembo 30 wanaoongoza makundi 30 katika mfumo wa Ikolojia wa Ruaha wa Rungwa, kola maalumu zenye vifaa vinavyorekodi mienendo yao ndani na nje ya hifadhi. Mratibu wa SPANEST Godwell Ole Meing’ataki anasema; “teknolojia hiyo inawezesha kupata taarifa za kina juu ya mienendo ya tembo katika mifumo mbalimbali ya ikolojia nchini zitakazosaidia kubainisha maeneo ya shoroba na mitawanyiko kwa ajili ya ulinzi wa tembo.”
Mtafiti Mwandamizi wa WEC, Dk Alfred Kikoti anasema kola hiyo inawezesha kujua maisha ya kila siku ya tembo. “Kola inamsaidia askari wa wanyamapori kufuatilia usalama wa tembo, kwani kinwaonesha walipo, wanapopita, kasi ya kutembea, sehemu wanazojificha, wanazokunywa maji, wanazopumzika, kama wamekufa, kujeruhiwa au wamehama hifadhi,” anasema.
HabariLeo

Related

Picha 2052181726626583951

Post a Comment

emo-but-icon

Follow Us

Comments

Video ya Siku

item